WAPINZANI WAPINGA HOTUBA YA JK BUNGE LA KATIBA

Wenyeviti wa vyama vya Upinzani vya
Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na
Chama cha NCCR-Mageuzi, jana usiku
walikutana ili kutoa kauli ya pamoja, kutokana
na hotuba ya ufunguzi wa Bunge kwa maelezo
kuwa tayari Rais amevuruga mchakato mzima
wa kupata Katiba Mpya.
Wakati viongozi hao wakikutana, Mwenyekiti wa
Chama cha DP Mchungaji, Christopher Mtikila
alisema, Rais ameingilia mchakato na kutoa
maelezo jinsi ya kuandika Katiba.
Wakizungumza na gazeti hili jana mara baada
ya hotuba hiyo, Freeman Mbowe, James Mbatia
na Profesa Ibrahim Lipumba, walisema
wameipokea kwa masikitiko makubwa hotuba
hiyo.
“Tunakwenda kujadili hotuba ya Rais na tutatoa
msimamo wetu,” alisema Mbowe.
Awali Katibu wa muda wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Julius Mtatiro alisema Rais
Jakaya Kikwete amevuruga mchakato wa
Katiba, kwani walitarajia angetumia mamlaka
yake kama Rais kuwaunganisha.
“Rais tulitarajia angeongea kama mkuu wa nchi,
lakini amezungumza kama Mwenyekiti wa CCM
na kutoa msimamo juu ya muundo wa
Muungano jambo ambalo hatukulitegemea,”
alisema Mtatiro.
Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni sawa na
mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato
mzima.
Hofu ya kuvunjika Bunge
Wakizungumza nje ya Bunge, baadhi ya
wajumbe wameeleza kuwa hotuba ya Rais
Kikwete kama ikitekelezwa uwezekano wa
kupata Katiba Mpya utakuwa mgumu.
Mjumbe Luhaga Mpina alisema kwa jinsi rasimu
ilivyoandikiwa na kama muundo wa serikali
mbili ukipita basi rasimu ya Katiba itabidi
iandikwe upya.
“Rasimu yote imetengenezwa kwa mfumo wa
serikali tatu sasa hapa kuna hatari ya Bunge
kukwama ,” alisema.
Mtatiro kwa upande wake alisema sasa kuna
hofu ya kushindwa kupatikana Katiba Mpya
kwani Rais amewachanganya wajumbe na
kama watapitisha maoni yake itabidi rasimu
kuandikwa upya.
Mjumbe Mustapha Akoonay, alisema
upatikanaji wa katiba upo shakani kwani sasa
upinzani utakuwa mkubwa juu ya muundo wa
muungano.
“Kwa sasa nadhani itabidi turudi upya kwa
wananchi kupata kura ya maoni juu ya
muundo wa muungano,” alisema.
Lucy Owenya alisema Rais amegeuza mkutano
wa Bunge kuwa ni mkutano wa Chama Cha
Mapinduzi, kwani ameshindwa kabisa kutoa
mwelekeo wa nchi na badala yake ametoa
msimamo wa CCM.
“Kutokana na hili, naamini kabisa Bunge
halitakuwapo na ni bora iwe hivyo kwa kuwa
amejibu hotuba ya Warioba na kwa maana hiyo
amepingana na mawazo ya wananchi.”
Godbles Lema alisema kuwa Rais hakuja
kuhutubia taifa bali alikuja kufanya semina na
kujibu hotuba ya Warioba.
Mjumbe huyo ambaye ni mbunge wa Arusha
Mjini alionyesha shaka kuwa baada ya muda
wa wiki tatu hakutakuwa na Bunge la Katiba
kwa kuwa wako baadhi ya watu ambao
hawatakubali kilichofanywa na Rais Kikwete.
“Waliochukua fedha ni vyema wakaenda
kumalizia nyumba zao kwa kuwa kiongozi wetu
amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafurahisha
wanaCCM lakini kwa Watanzania hatutakubali,”
alisema Lema.
John Cheyo alisema, “Mimi ninachokiona ni
maridhiano tu, suala la kufumua rasimu halinipi
shida kwa kuwa vitu vyote vinavyoletwa
bungeni huwa ni mali ya Bunge na hivyo
tutafanya tunavyoona sisi inafaa.”
Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuwa kosa
kubwa ambalo lilifanywa na upinzani ni
kukubali na kuruhusu Jaji Warioba atangulie
kuwasilisha rasimu yake akasema hilo ndilo
lililowagharimu.
Alitaka Bunge livunjwe mara moja ili warudi
kwa wananchi wakaamue na kuwahukumu
kutokana na kile ambacho walikifanya katika
Bunge ambalo kwa maoni yake wamekula
fedha za walipa kodi bure.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa
aliipongeza hutuba ya Rais Jakaya Kikwete ya
uzinduzi wa Bunge la Katiba.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge la
Katiba, alisema kwa kifupi hotuba ya Rais
Kikwete ni nzuri. Lowassa alitoa kauli hiyo,
wakati akitoka nje ya Bunge, muda mfupi
baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza hotuba
ya uzinduzi wa Bunge hilo.

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.