Kashfa Saba Nzito Nchini Zilizotugharimu na Kututia Aibu
Dar es Salaam. Serikali imepoteza zaidi ya
Sh362.9 bilioni kutokana na baadhi ya kashfa
kubwa za ufisadi na operesheni mbalimbali
zilizoligharimu taifa tangu uhuru.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini taifa
kukumbwa na kashfa mbalimbali za upotevu
wa fedha au kuanzisha mipango ambayo
utekelezaji wake ulisababisha maumivu kwa
wananchi na hakuna awamu ya uongozi wa
Serikali iliyokwepa hali hiyo.
Kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius
Nyerere aliyeiongoza nchi toka mwaka 1961
ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali Hassan
Mwinyi (1986-1995), Rais Benjamin Mkapa
(1995-2005) na Rais Jakaya Kikwete (2005-hadi
sasa), kumeibuka kashfa mbalimbali, saba
zikiwa kubwa na kulitikisa taifa.
Kashfa na operesheni saba kubwa zilizotikisa
taifa ni pamoja na Operesheni Uhujumu
Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha
Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity
Import Support – CIS) na Kashfa ya Rada.
Nyingine ni ufisadi Akaunti ya EPA, kashfa ya
Richmond, Operesheni Tokomeza Ujangili na ile
ya uchotaji mabilioni katika akaunti ya Escrow.
Operesheni Uhujumu Uchumi
Mwaka 1984 Serikali ilianzisha Operesheni
Uhujumu Uchumi, iliyoongozwa na Waziri Mkuu
wa wakati huo, Edward Sokoine ili kutaifisha
mali ambazo baadhi ya watu walidaiwa
kujipatia kwa njia isiyo halali.
Operesheni hiyo ilishuhudia baadhi ya
watuhumiwa wakimwaga fedha mitaani na
majalalani, huku wengine wakitupa mali kuhofia
kutiwa kwenye mkono wa sheria.
Hata hivyo, katika operesheni hiyo baadhi ya
watendaji wa Serikali ambao hawakuwa
waaminifu, waliitumia nafasi hiyo vibaya
kutaifisha mali za baadhi ya watu, ambao
hawakuwa wahujumu uchumi.
Zoezi hilo lilisababisha wananchi kadhaa hasa
vijijini kuwekwa ndani na wengine kuachwa
maskini baada ya kunyang’anywa mali zao
ikiwamo mifugo na mashine za kusaga nafaka,
kwa kudaiwa kuwa walizipata kwa njia isiyo
halali.
Mfuko wa Commodity Import Support (CIS)
Miaka 24 baadaye yaani mwaka 2008, liliibuka
sakata jingine lililokuwa na harufu kubwa ya
ufisadi wa mabilioni katika Mfuko wa
Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi
(Commodity Import Support – CIS).
Sakata hilo liliwahusisha baadhi ya wanasiasa,
wafanyabiashara maarufu nchini na wizara
kadhaa za Serikali ya Muungano na ile ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Kupitia mfuko huo, vigogo hao walichota zaidi
ya Sh200 bilioni kwa kivuli cha uagizaji bidhaa
kutoka nje ya nchi.
Mfuko huo wa CIS, ulianzishwa katika miaka ya
1980, ambapo baadhi ya nchi wafadhili ikiwamo
Japan, zililenga kuipatia Tanzania fedha za
kigeni za kununulia malighafi, vyombo vya
usafiri wa barabara, vifaa vya kilimo, ujenzi na
vingine mbalimbali. Mpango huo ulioanzishwa
na Serikali uliendelea hadi mwanzoni mwa
miaka 2000, ambapo nchi hizo wahisani
ikiwamo Japan, Uingereza, Uholanzi, Saudi
Arabia, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Sweden na
Denmark zilikuwa zikiipatia Serikali fedha za
kigeni ili kuimarisha sekta za biashara.
Wizara zilizotajwa katika orodha ya wadeni wa
CIS ni pamoja na iliyokuwa ya Mawasiliano na
Uchukuzi, Wizara ya Kazi, Wizara ya Kilimo,
Wizara ya Maji na Wizara ya Mambo ya Ndani
kwa Tanzania Bara, wakati Zanzibar zinatajwa
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara
ya Maji.
Rada
Mwaka 2011 Serikali ilikumbwa na jinamizi la
ufisadi kwa mara nyingine. Safari hii uliibuka
ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi
wa rada kuukuu kutoka Kampuni ya BAE
Systems ya Uingereza. Ununuzi wa rada hiyo
unatajwa kutofuata taratibu sahihi, uliligharimu
taifa Sh29.5 bilioni, wakati gharama halisi
ilikuwa Sh21 bilioni.
Serikali ya Uingereza iliamua kurudisha fedha
hizo kama chenji, huku ikisisitiza kuwa
watuhumiwa wote wa hapa nchini waliohusika
na ununuzi wa rada hiyo mtumba, washitakiwe
Tanzania au Uingereza kutokana na kubainika
dosari kwenye ununuzi huo.
Wakati Uingereza ikitaka watuhumiwa hao
wafikishwe mahakamani, mtandao wa Wikileaks
unaosifika kwa kufichua siri za ndani ya mataifa
mbalimbali duniani, ulibaini kuwepo kwa
harakati nchini za kutowafikisha mahakamani
wahusika wa ufisadi huo.
EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa
mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni
ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), ambapo
vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota
zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti hiyo.
Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika
walitajwa kutumia vivuli vya siasa katika
kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki wa
nyaraka hizo.
Richmond
waka 2006 baada ya Rais Jakaya Kikwete
kuingia madarakani kulitokea tatizo kubwa la
uhaba wa umeme.
Hapo ndipo Serikali ilipoanza kufanya mikakati
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za
dharura za kutatua tatizo hilo.
Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa
alikuwa mstari wa mbele katika mikakati hiyo
ndipo Kampuni ya Richmond Development (LLC)
ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura
na kuliuzia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini
Tanesco.
Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa kampuni
hiyo haikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme
kama ilivyodhaniwa, badala yake kulikuwa na
michezo michafu iliyofanyika kwa masilahi ya
wafanyabiashara na baadhi ya viongozi wa
Serikali.
Mwaka 2007, sakata hilo lilifika bungeni na
aliyekuwa Spika wakati huo, Samuel Sitta
aliunda kamati iliyokuwa chini ya mbunge wa
Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ili kuchunguza
suala hilo.
Kamati hiyo ilichunguza sakata hilo na kutoa
taarifa ilionyesha kuhusika kwa viongozi wa juu
wa Serikali akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu
Edward Lowassa na kusababisha kiongozi huyo,
kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili kung’oka
madarakani.
Waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati
na Madini kwa vipindi tofauti, ambao ni Naziri
Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.
Operesheni Tokomeza Ujangili
Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanzishwa na
Serikali kupambana na ujangili wa wanyama
nchini mwaka jana iliwang’oa madarakani
mawaziri wanne ambao wizara zao zilielezwa
kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa
operesheni hiyo.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa
bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua
uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa
mashauriano akiwa nchini Marekani.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya
kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na
michango ya wabunge wengi ni Waziri wa
Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki na Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo
David Mathayo.
Operesheni hiyo inadaiwa kukiuka haki za
binadamu ikiwamo watu 13 na askari sita
kuuawa, utesaji wa kutisha wa watuhumiwa,
ubakaji, rushwa na uporaji wa mali za
wananchi.
Akaunti ya Esrow
Wakati kashfa ya Richmond haijasahaulika,
mapema mwaka huu imeibuka kashfa ya
upotevu wa mamilioni ya fedha kwenye
Akaunti ya Esrow katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Kashfa hiyo inayolitikisa Bunge na Serikali sasa,
imetajwa kuwa ni mwendelezo wa jinamizi la
kashfa ikiwa ya saba kubwa kulikumba taifa
hadi sasa.
Akaunti hiyo iliyokuwa na zaidi ya Sh200 bilioni,
ilifunguliwa wakati kukiwa kuna mgogoro wa
kisheria baini ya wabia wa zamani wa IPTL (VIP
Engeneering and Marketing na Mechmar
Corporation ya Malaysia) kwa upande mmoja,
Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT,
kwa upande mwingine.
Wadau kwenye akaunti hiyo hawakupaswa
kuchukua kitu chochote hadi pale mgogoro
utakapotatuliwa. Hata hivyo, kitita hicho cha
fedha kilichotwa.
Wazungumza
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
(OUT), Emmanuel Mallya alisema matukio ya
ufisadi yanaongezeka nchini kutokana na
Serikali kushindwa kuweka bayana hatua
zinazopaswa kuchukuliwa watu wanapatikana
na makosa hayo, ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema kila mara wizi wa fedha za umma
unapotokea, Serikali hupata kigugumizi
kuwawajibisha wahusika, hatua inayowafanya
watu wengi kuamini kushindwa kwao
kunatokana na woga wa kutekeleza azma zao.
“Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo
fulani, kuna kulindana sana, lakini kama wote
wangechukuliwa hatua za wazi pengine ufisadi
usingekuwa wa kiwango cha juu namna hii,”
alisema.
Mhadhiri
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
(UDSM) Faraji Christoms, alishauri wenye
dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa
wanatakiwa kujitathmini upya.
Alitaja maeneo yanayohitajika kufanyiwa
tathmini kuwa ni uzalendo kwa taifa, elimu kwa
maana ya uelewa wa mambo ya kisheria, lugha
za kimataifa na umakini wakati wa majadiliano
ya kimataifa na wanaposoma mikataba ya aina
hiyo.
No comments