Lissu Arusha Kombora Lingine kwa Mawaziri
Dodoma. Waziri wa Maji, Profesa Jumanne
Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge, jana
walituhumiwa kutumia vibaya nafasi zao kwa
kuweka fedha nyingi za miradi ya maji katika
maeneo wanakotoka, huku sehemu zenye
matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha
kiduchu.
Ilielezwa bungeni jana kuwa Profesa Maghembe
ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro,
wizara yake imetenga Sh1.4 bilioni kwa ajili ya
miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba
ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo
katika Wilaya ya Ikungi, Singida.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji jana,
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),
Tundu Lissu alihoji kile alichokiita upendeleo wa
wazi katika ugawaji wa fedha za maji, unaoipa
kipaumbele baadhi ya mikoa wanakotoka
mawaziri.
Pia aliitaja Wilaya ya Makete, Njombe
anakotokea Dk Mahenge ambaye amewahi
kuwa Naibu Waziri wa Maji kuwa imetengewa
Sh1.9 bilioni na kusema: “Upendeleo wa aina
hii haufai kwa sababu utaleta matatizo na siyo
haki hata kidogo.”
“Profesa Maghembe atueleze sababu za
kutenga bajeti hii kwa upendeleo, huku mikoa
isiyokuwa na vyanzo vya maji, mito ya kudumu
na mabwawa ya maana imepewa bajeti kidogo
ikilinganishwa na ile yenye mifumo mizuri ya
maji,” alisema Lissu.
Alisema licha ya Profesa Maghembe katika
hotuba yake kutaja mikoa ya
Dodoma, Singida,
Simiyu na Shinyanga kuwa inakabiliwa na
upungufu wa maji, imetengewa kiasi kidogo cha
fedha, huku mikoa inayopata mvua za kutosha
na vyanzo vya uhakika vya maji ikitengewa
mabilioni ya fedha.
“Dodoma imetengewa Sh7.2 bilioni, Singida
Sh3.2 bilioni, Shinyanga Sh3.2 bilioni na Simiyu
Sh2.8 bilioni, wakati mikoa yenye vyanzo vya
maji na mvua za kutosha imetengewa fedha
nyingi; mfano ni Tanga Sh10.7 bilioni,
Kilimanjaro Sh6.3 bilioni, Mbeya Sh9.2 bilioni
na Mtwara Sh7.5 bilioni,” alisema.
Lissu alisema hali hiyo inaweza kutafsiriwa
kuwa mawaziri hao wanatumia mamlaka yao
kujipendelea na kuhoji kama huo ndiyo
utaratibu wa Serikali ya CCM...
“Kama utaratibu
wa mgawanyo wa fedha ndiyo huu sisi
tunaotoka mikoa yenye ukame tutapataje maji?”
Jana Profesa Maghembe aliendelea kuwa katika
wakati mgumu, baada ya kuandamwa na
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
ambaye alimwita kuwa ni mzigo kutokana na
kutokutolewa kwa fedha za miradi ya maji.
Mnyika alionyesha kushangazwa na wabunge
wenzake kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo,
licha ya kuwa ndogo na fedha za miradi
zimekuwa hazitolewi kama inavyotakiwa.
“Kwa kufanya hivi sidhani kama tunamsaidia
Profesa Maghembe ambaye ni CCM. Fedha
zilizotengwa mwaka jana kuisaidia wizara hii
hazijatoka na za bajeti hii hazitatoka kwa
kiwango cha kuwezesha utekelezaji. Namna
bora ya kumsaidia ili viongozi wa CCM
wasiendelee kumwita mzigo ni kuikataa bajeti
hii ili Serikali irudi mezani na kujiuliza.”
No comments